Phinias Bashaya,Bukoba
Wakazi wa mji wa Bukoba wameonyesha hofu ya kulipuka kwa magonjwa ya kuambukiza kutokana na uchafuzi wa maji ya mto Kanoni yanayotumiwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya nyumbani.
Hofu hiyo imekuja kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ambapo uchafu mwingi husombwa na maji ya mvua na kuingia katika mto huo unaopita katikati ya mji wa Bukoba.
Wakitoa malalamiko yao kwa nyakati tofauti,baadhi ya wananchi wa Kata za Bakoba ,na Hamugembe wamesema mto huo umejaa uchafu mwingia ambao unaweza kuhatarisha maisha yao kutokana na baadhi ya wananchi kutegemea maji yam to huo.
Mmoja wa wananchi hao Japhet Kyoma alisema hali mbaya ya uchafu inayoukabiri mto huo kwa kwa sasa inahatarisha maisha ya wananchi na kuwa na uwezekano mkubwa wa kutokea kwa magonjwa ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu.
Pia mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Kamazima alidai uchafu mwingi unaozalishwa na wananchi wanaozunguka mto huo hurushwa ndani ya maji badala ya kuupeleka katika maeneo maalmu yaliyotengwa na Manispaa ya Bukoba.
Pia alisema wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi zilizopo karibu na mto Kanoni wako katika hatari zaidi ya kupata magonjwa ya kuambukizwa ambao kila mara huonekana wakichota maji katika mto huo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya shuleni ikiwemo umwagiliaji wa maua.na usafi.
Aidha baadhi ya wananchi walilalamikia ujenzi holela unaoendelea kando yam to huo kuwa unachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mto huku Manispaa ikilalamikiwa kwa kufumbia macho ujenzi unaoendelea.
Pia baadhi ya wananchi waliwataka viongozi wa Manispaa ya Bukoba kudhibiti hali hiyo inayoelekea kuhatarisha afya zao na kupendekeza kununuliwa kwa gari la kufyonza maji taka tofauti na ilivyo sasa.
No comments:
Post a Comment